27 Mei 2021 - 12:01
Biden ataka Congress ichukue hatua baada ya watu wengine 8 kuuawa kwa risasi Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani amelitaka Bunge la Kongresi la nchi hiyo litekeleze hatua za kukomesha janga la uhalifu wa silaha za moto nchini humo, masaa machache baada ya Wamarekani wanane kuuawa katika tukio jingine la ufyatuaji risasi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Sanjari na kuagiza bendera zipepee nusu mlingoti katika Ikulu ya White House kwa mara nyingine tena kutokana na mauaji hayo, Biden amesema kila uhai unaokatizwa kwa risasi, unaacha ufa kwa taifa la Marekani, na kwamba kuna haja ya kuchukua hatua zaidi za kukomesha ukatili huo wa umwagaji damu kiholela.

Jana Jumatano, watu wasiopungua wanane waliuawa katika tukio la ufyatuaji risasi lililotokea katika mji wa San Jose ulioko kwenye kaunti ya Santa Clara jimbo la California nchini Marekani.

Polisi ya California imesema mfanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri ya Valley katika eneo hilo aliyetekeleza unyama huo ameuawa pia. 

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, watu wasiopungua 10 waliuawa katika tukio la ufyatuaji risasi lililotokea katika mji wa Boulder ulioko kwenye jimbo la Colorado nchini Marekani.

342/